Trusted since 2008
Study resources on Kenyaplex

Get ready-made curriculum aligned revision materials

Exam papers, notes, holiday assignments and topical questions – all aligned to the Kenyan curriculum.

Soma makala yafuatayo kisha ujibu maswali. Ni dhahiri shahiri kwamba uharamia umechipuka kama desturi na mfumo wa maisha katika siku za hivi karibuni. Janga hili limeshamiri...

Soma makala yafuatayo kisha ujibu maswali.
Ni dhahiri shahiri kwamba uharamia umechipuka kama desturi na mfumo wa maisha katika siku za hivi karibuni. Janga hili limeshamiri hususan pembeni mwa bara la Afrika na kanda ya Afrika Mashariki.Taarifa za uharamia zimetawala vyombo vya habari, kiasi cha kwamba haipiti siku bila kuripotiwa visa vipya vya matendo haya mabovu ambayo yanaweza tu kumithilishwa na uhayawani.Matukio haya yamewalimbikizia mabaharia na nchi husika, simanzi na masaibu yasiyoweza kutiwa kwenye mizani.
Yumkini tatizo hili halitokei pasi na kumotishwa na kitita kikubwa cha fidia kinachodaiwa na maharamia hawa. Aghalabu, suala hili lahusishwa pakubwa na azma na ari ya kuendeleza ujambazi wa kimataifa sawia na ulipuaji wa bomu mijini Nairobi na Dar es Salaam mnamo Agosti 7,1998, na tukio la Septemba 11, mwaka wa 2001 kule Marekani.Maafa na uharibifu wa mali si hoja, la mno kwa maharamia ni kutosheleza matakwa yao. Kwa upande mwingine, ukosefu wa tawala-wajibika katika maeneo kunakotokea unyama huu ni thibitisho tosha la mazingara yanayowezesha na kuruhusu kuchipuka kwa janga hili.
Mchipuko wa baa la uharamia umelengwa jamii ya kimataifa ambayo ni mhudumu mkuu wa harakati za kusitisha majanga makubwa kama vile njaa, umaskini na magonjwa yaliyosheheni pakubwa barani. Bila shaka, hili ni suala linalosawisishwa na ‘kinyume mbele’. Maharamia wanatishia utangamano wa kimataifa wanapotibua usafiri wa abiria na shehena zinazoelekezwa sehemu tofauti ulimwenguni.
Matumizi ya kidiplomasia na mashauriano hayaelekei kuzalisha matunda katika juhudi za kudhibiti uharamia. Zaidi ya hayo, matumizi ya nguvu yahusishayo mashambulizi pamoja na maharamia kufunguliwa mashtaka nchini Kenya na Ufaransa kunaelekea kuzipiga jeki juhudi za uharamia ulimwenguni.Aidha, utawala wa nchi kunakochipuka uharamia haujajizatiti kuharamisha doa hili linalotisha ustawi wa kimataifa.
Mathalan, ni jambo lisilopingika inapobainika kuwa uharamia umedumaza biashara ya kimataifa, hali inayochangia upungufu na ucheleweshaji wa bidhaa muhimu zinazoendeleza ustawi wa uchumi. Dosari hii inaelekea kukwamiza mojawapo wa malengo ya maendeleo ya milenia yanayosisitiza uimarishaji na ushirikiano wa maendeleo na upanuzi wa masoko ulimwenguni. Harakati za kitalii katika kanda ya mashariki ya bara la Afrika zimehujumiwa. Ni muhali kwa utalii kustawi kwenye maeneo yaliyo na tishio la usalama. ltakumbukwa bayana kwamba watalii hawasafiri tu kwa ndege bali hata kwa meli.
Jitihada za kuweka laini za mawasiliano chini ya bahari ili kurahisisha na kupunguza gharama za mtandao ulimwenguni ni ndoto ambayo haijatimia hadi hivi sasa, kufuatia juhudi za maharamia katika bahari ya Hindi. Kwa mujibu wa hali hii, mawasiliano mepesi na nafuu yasitarajiwe hivi karibuni. Licha ya hayo, shughuli za uvuvi na biashara nyenginezo kwenye kanda ya mwambao zimetiliwa shaka si haba.
Itabidi mikakati na suluhisho la kudumu liweze kupatikana ili vitendo vya uharamia viweze
kusitishwa.

MASWALI

(a) Kwa nini uharamia umetamalaki ulimwenguni?

(b) Fafanua dhana ya ‘kinyume-mbele’ kwa mujibu wa taarifa hii.


(c) Uharamia unaelekea kumtia hofu mwandishi. Fafanua.


(d) Thibitisha kuwa Kenya imeathirika pakubwa kutokana na vitendo vya uharamia




(e) Ukirejelea kifungu, eleza maana ya:
(i) uharamia ………………………………………………………………………………….
(ii) mtandao …………………………………………………………………………………
(iii) mwambao ………………………………………………………………………………

Answers


Peter
a)
(i) Pesa au fidia wanazolipwa maharamia.
(ii) Ari ya kuendeleza ujambazi wa kimataifa
(iii) Ukosefu wa utawala wa kuwajibika katika sehemu/nchi kunakotokea uharamia

b) Uharamia unaotokea barani Afrika umeelekezewa jamii ya kimataifa ambayo ni mhusika mkuu wa kuinusuru Afrika kutokana na njaa, magonjwa na umaskini.
(i) Matumizi ya diplomasia na mashauriano hayajafaulu katika kumaliza uharamia ulimwenguni
(ii) Matumizi ya nguvu (mashambulizi na mashtaka) yanaonekana kuendeleza uharamia.
(iii) Utawala/ uongozi wa mataifa husika haujajizatiti kuuharamisha uharamia.
d)
(i) Uharamia umedumaza biashara kutokana na upungufu na ucheleweshaji wa bidhaa muhimu zinazohitajika nchini.
(ii) Shughuli za kitalii zinahujumiwa
(iii) Kucheleweshwa kwa uwekaji wa nyaya/ laini za kuwezesha urahisi na wepesi wa
mawasiliano ulimwenguni.
(iv) Uvuvi pamoja na shughuli nyingine zinazotendeka mwambao haziendelezwi ipasavyo.
e)
(i) Wizi, ujambazi au unyang’anyi wa baharini kwa kutumia nguvu.
(ii) Mfumo wa mawasiliano yaunganishayo ulimwengu kwa matumizi ya tarakilishi au simu
za rununu.
(iii) Sehemu ya nchi iliyo karibu na bahari; pwani.



Musyoxx answered the question on February 22, 2018 at 16:23

Answer Attachments

Exams With Marking Schemes

Related Questions