Get premium membership and access revision papers, questions with answers as well as video lessons.
Got a question or eager to learn? Discover limitless learning on WhatsApp now - Start Now!

Kcpe 2009 Kiswahili Question Paper

Kcpe 2009 Kiswahili 

Course:Kiswahili

Institution: Kcpe question papers

Exam Year:2009



KCPE 2009
KISWAHILI
Soma vifungu vifuatavyo. Vina nafasi 1 mpaka 15. Kwa kila nafasi umepewa majibu manne hapo.
Chagua jibu lifaalo Zaidi kati ya yale uliyopewa.
Kipepesi ni njia mojawapo—1—sana siku hizi—2—mawasiliano. Njia---3---hutumika Zaidi ofisini.
---4---ni kati ya matokeo ya maendeleo ya kiteknonojia—5—dunia kuwa duara ndogo---6---walimwengu huweza---7---kwa njia rahisi.
1. A. Zilizotumika
B. Zinazotumika
C. Inayotumika
D. Iliyotumika

2. A. Katika
B. Kuhusu
C. Ndani ya
D. Mbali na

3. A. Hiyo
B.Hizi
C. Hizo
D. Hii

4. A. Ama
B. Aidha
C. Na
D. Au

5. A. Iliyoiwezesha
B. Yaliyowezesha
C. Iliyoliwezesha
D. Yaliyoiwezesha

6. A. Amabayo
B. Ambao
C. Ambapo
D. Ambalo
7. A. Kuwasiliana
B. Kuwasilisha
C.Kuwasilishwa
D. Kuwasilishiana

Kuweko kwa---8---ya UKIMWI---9—swala la mjadala tena---10—ni watoto wachanga tu ambao---11---ukweli huu—12--. Hata hivyo, hatuwezi kupoteza tumaini---13---. Wanasayansi wa humu nchini na kwingineko duniani---14---wanaendelea na---15---wao kutafuta tiba.
8. A. Magonjwa
B. Maradhi
C. Uwele
D. Ukongo

9. A. Ni
B. Si
C. Ndio
D. Sio

10. A. Kwa vile
B. Angalau
C. Ikiwa
D. Labda

11. A. Hawaujui
B. Wanaujua
C. Huujua
D. Hawakuujua

12. A. Mchungu
B. Mkubwa
C. Ukubwa
D. Uchungu

13. A. Pia
B. Kweli
C. Kabisa
D. Hakika
14. A. Walikuwa
B. Wangekuwa
C. Wanakuwa
D. Wangali
15. A. Upelelezi
B. Udodosi
C. Uamuzi
D. Utafiti

Kutoka swali la 16 mpaka 30, chagua jibu lililo sahihi.
16. “Ka” imetumiwaje katika sentensi:
Mvulana aliwasili nyumbani, akavua nguo, akafululiza jikoni, akala?
A. Kuonyesha hali ya kuendelea kwa matukio.
B. Kuonyesha hali ya kufuatana kwa matukio.
C. Kuonyesha hali ya masharti.
D. Kuonyesha hali ya wakati uliopita.
17. Kukanusha sentensi hii:
Mahali kuliko na gharika kwahitaji msaada.
A. Mahali kuliko na kiangazi hakuhitaji msaada.
B. Mahali kuliko na kiangazi kwahitaji msaada.
C. Mahali kusiko na gharika kwahitaji msaada
D. Mahali kusiko na gharika hakuhitaji msaada.
18.Chagua jawabu lisilo sahihi.
A. Paa ni mnyama.
B. Paa ni kwenda juu.
C. Paa ni sehemu ya mbele ya uso.
D. Paa ni sehemu ya juu ya nyumba.

19. Geuza katika usemi wa taarifa:
Mwalimu aliwaambia wanafunzi, “Tutakamilisha shughuli ya kudurusu kwa kufanya mtihani muhula huu.”
A. Mwalimu aliwaarifu wanafunzi kuwa wangekamilisha shughuli ya kudurusu kwa kufanya mtihani muhula huo
B. Mwalimu aliwaarifu wanafunzi kuwa wangekamilisha shughuli ya kudurusu kwa kufanya mtihani muhula huu
C. Mwalimu aliwaarifu wanafunzi kuwa watakamilisha shughuli ya kudurusu kwa kunfanya mtihani muhula huu.
D. Mwalimu aliwaarifu wanafunzi kuwa watakamilisha shughuli ya kudurusu kwa kufanya mtihani muhula huo.
20. “Wa” imetumikaje katika sentensi:
Uzi mweupe wa kushonea umenunuliwa?
A. Kuonyesha kumiliki.
B. Kuonyesha matumizi.
C. Kuonyesha kitenzi.
D. Kuonyesha hali.
21. Panga vifungu vifuatavyo kuunda sentensi sahihi.
(i) Kuonyesha kumiliki.
(ii) Kila tukipanda.
(iii)Mahindi.
(iv) Na kuyala
(v) Kuchakulo
A. (ii), (iii), (v), (i), (iv)
B. (i), (iv), (iii), (v), (ii)
C. (ii), (iii), (iv), (v), (i)
D. (i), (v), (ii), (iii), (iv)

22. Nomino kutokana na kitenzi ‘nyamaa’ ni:
A. Nyamazia
B. Kunyamavu
C. Nyamaza
D. Unyamavu

23. Zabuni ni:
A. Kuuza kwa kuongezea bei.
B. Kuuza kwa kushindania bei.
C. Kuuza kwa rejareja.
D. Kuuza kwa kukopesha.

24. Ni methali ipi iliyo na maana tofauti na maelezo haya? Ukisoma ukurasa mmoja mmoja utakamilisha kitabu chote.
A. Bandu bandu huisha gogo.
B. Chovya chovya humaliza buyu la asali.
C. Tone na tone bahari hujaa
D. Chururu si ndo ndo ndo.

25. Chagua kiwakilishi katika sentensi:
Huyu anaupinga vikali ufisadi.
A. Ufisadi
B. Vikali
C. Anaupinga
D. Huyu
26. Mazingira, machozi na mate ni nomino katika ngeli ya
A. YA-YA
B. I-ZI
C. LI-YA
D. U-YA

27. Chagua kiambishi kifaacho kujazia pengo:
Farasi hata----shinda nyumbe.
A. I
B. Li
C. M
D. Zi
28. Chagua neno lenye maana sawa na minghairi ya:
A. Mradi
B. Pasipo
C. Isipokuwa
D. Bali.

29. Jibu la kitendawili:
A. Afahamu kuchora lakini hajui achoracho ni:
A. Mjusi
B. Kobe
C. Konokono
D. Nyoka

30. Chagua sentensi ambayo imetumia kihisishi kifaacho.
A. Simile! Mpishe mwenye mzigo.
B. Pole jamani! Mmepata afueni nyote
C. Alhamdulilahi! Mali yote imeporwa.
D. Pukachaka! Amependekeza suluhisho nzuri.

Soma kifungu kifuatacho kasha ujibu maswali 31-40.
Jamii thabiti huhitaji misingi madhubuti ya makuzi ya watoto.
Hoja ya wazazi isiwe tu kujitafutia mali kiholela bali iwe ni kuwatambua warithi wa mali inayotafutwa. Hii ndiyo maana wazazi wengi leo hujikusuru kuisimamisha misingi ya malezi bora ya watoto kwa kuwasomesha.
Kumsomesha mtoto tu bila msingi wa nidhamu ni kama kulijenga jumba la ghorofa bila msingi imara na kuporomoka kwake si ajabu.Vijana wanapaswa kuelewa umuhimu huu ili wawe tayari kuupokea uongozi na urathi wa jamii.
Misingi madhubuti ya kinidhamu hujengwa tangu watoto wakianza kutambua mambo. Kungoja mpaka mtoto awe mkubwa ndipo aanze kufunzwa maadili ni kama kujaribu kumkunja samaki akiwa tayari amekomaa na kuwa mkavu; udongo tuuwahi uli maji.

Hapo kale mambo yalikuwa tofauti. Mtoto aliweza kukosolewa na mtu yeyote yule hata kama alikuwa ni mpita-njia. Watoto walikuwa ni wa jamii, hulka zao zilionekana mapema kama vile nyota njema zionekanavyo alfajiri. Watoto walikuwa wakitenda mambo huku wakijihisi kuwa wanakodolewa macho na jamii. Hisia hizo ziliwafanya watoto kujichunguza, kujiasa na kutenda kila jambo kwa tahadhari. Watoto waliwaheshimu watu wazima bila kushurutishwa, hali ambayo ilijenga uhusiano mzuri katika jamii.
Mtoto afunzwaye adabu ipasavyo kawaida hawezi kutetereka popote alipo, iwe shuleni au nyumbani.
Mtoto kama huyo kufanywa zumbukuku na watovu wa nidhamu sio rahisi, bali ataweza kuchukua nafasi ya walimu na wazazi kuyapitisha maadili mwafaka kwa wenzake. Mtoto huyo hukuza mbegu bora katika jamii. Yeye hujistahi, huwa na bidii na uvumilivu mwingi. Wazazi wakilea watoto wa aina hii na wawaongezee mafunzo ya kidini, jamii itakuwa na uhakika wa kuwa na warithi bora. Watoto hao wataweza kuchangia pakubwa katika maendeleo ya nchi kwa jumla.
Ipo haja kubwa sasa ya kuacha kung’ang’ania kasumba na tamaduni za kigeni katika malezi.
Tuache ubaguzi, uvivu na ubinafsi ili kuwapa watoto mifano bora na miangaza ya kuwakuza kifikira, kielimu,kiuchumi na kitamaduni. Jamii isipuuze kutoa michango yake katika urekebishaji wa watoto. Mathalani, ni makosa kuacha kumkosoa mtoto atendaye mambo ya kuyahatarisha maisha yake nay a wenzake.
Watoto hata nao wana jukumu katika kuyaimarisha maisha yao. Wanapaswa kuziepuka tabia zote mbaya hata ikiwa hawapewi misingi makwao. Wanaweza kuziiga jamii nyofu kinidhamu hata ikiwasio wazazi wao na kuyatupilia mbali mambo maovu ambayo yanawazunguka katika jamii. Ni vizuri kuwa urithi bora ni ule wa kuiga tabia nzuri, bidii na kupata elimu yenye manufaa.

31. Kulingana na kifungu, misingi bora ya watoto hukuzwa kwa:
A. Wazazi kutotafuta mali na kuwasomesha warithi
B. Kuujua umuhimu wao na kuwapa maelekezi
C. Kuwa na misingi madhubuti shuleni
D. Kufunza watoto kujikusuru kiuchumi.

32. Maana ya “kuporomoka kwake si ajabu” ni:
A. Haishangazi ikiwa ghorofa itaanguka
B. Malezi ya watoto kuharibika si kazi
C. Wazazi kushindwa malezi si ajabu
D. Ni rahisi jamii kupoteza warithi

33. Amekomaa na kuwa mkavu; huweza kulinganishwa na:
A. Ugumu wa malezi bora
B. Madhara ya ucheleweshaji wa kufunza nidhamu
C. Madhara ya ucheleweshaji wa masomo ya watoto
D. Ugumu wa kuwakosoa watoto.

34. Watoto wa zamani:
A. Walilelewa kwa ugumu
B. Waliwaogopa wazazi waliowalea
C. Walikomaa kwa haraka
D. Walilelewa kwa ushirikiano.

35. Watoto kuhisi kuwa wanatazamwa na jamii kuliwafanya waweze:
A. Kuithamini jamii Zaidi
B. Kuiogopa jamii majumbani
C. Kuwajibika katika jamii
D. Kurekebisha tabia katika jamii.

36. Kulingana na kifungu, ubaguzi katika malezi hutokea:
A. Wazazi wanapopuuza kurekebisha makosa ya watoto wengine
B. wazazi wanapoanza kuwasomesha watoto wao tu
C. Jamii inapoanza kuwakodolea watoto macho bila kuwasaidia
D. Vijana wanapopuuza ushauri wa wanajamii wengine.

37. Watoto hata nao wana jukumu katika kuyaimarisha maisha yao.
Methali inayoweza kutumiwa kujumuisha maneno haya ni:
A. Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo
B. Ukishikwa shikamana
C. Ukibebwa usilevyelevye miguu
D. Mtoto akibebwa hutazama kisogo cha nina.
38. Warithi bora katika hukuzwa kwa:
A. Malezi bora na elimu
B. Kuheshimiwa na wakubwa
C. Malezi ya kizamani
D. Kuaminiwa na jamii.

39. Maana ya “hawezi kutetereka” ni:
A. Hawezi kubabaika
B. Hawezi kupotoka
C. Hawezi kushawishika
D. Hawezi kutetemeka

40. Chagua neno lenye maana sawa na hujistahi kama lilivyotumiwa katika kifungu.
A. Hujisifu
B. Hujipenda
C. Hujiamini
D. Hujiheshimu.

Soma taarifa ifuatayo kasha ujibu maswali 41 mpaka 50.
Asubuhi hiyo Tundu aliamka akiwa mchovu wa mwili na roho. Ulikuwa mwanzo wa siku ambayo kwake Tundu ilifanana na zingine za awali kama shilingi kwa ya pili. Katu haingempa matumaini mapya. Usiku uliopita ulizongwa na hamaniko na mavune makubwa kutokana na shughuli za kutwa shuleni. Kutwa hii ilikuwa amepewa adhabu ya kupalilia shamba la shule baada ya kukosa kufanya zoezi la hesabu.
Ingawa kufanya adhabu kulikuwa mazoea yake Tundu, hii ya leo ilikuwa ya kipekee kwani hata baada ya kuikamilisha, mwalimu mkuu alimpa nyongeza;alihitajika kuyafanya mazoezi mengine mawili Zaidi na kumkabidhi mwalimu kesho yake asubuhi.
Tundu alijikokota kutoka kitandani kwa maumivu. Alijua kwamba hakuwa amekamilisha kazi aliyopewa na mwalimu mkuu. Fikira ya kumkabili mwalimu mkuu ilimtia fadhaa ya ajabu, ila alifahamu sababu ya fadhaa yake. Vituko vyake vilikuwa vimewakaba walimu koo. Alikuwa hahudhurii madarasa yake kwa desturi. Mara nyingi alitoka nyumbani alfajiri na mapema. Hata hivyo hakudiriki kufika shuleni; japo kwa kweli alikuwa akivaa sare za shule kuwasadikisha wazazi kuwa anaenda shuleni. Wazazi wake walipojuzwa na walimu kuhusu tabia hii, walipigwa na butwaa wasijue la kusema. Waliwaambia walimu kwamba kila siku Tundu alikuwa akiondoka akiwa amevaa sare kamili ya shule, na aliporejea nyumbani magharibi alifululiza chumbani kudurusu kazi yake. Laiti wangalijua kwamba Tundu alikuwa akivaa magwanda yake ya ‘kazi’ ndani ya sare za shule na pindi tu apoteapo kwenye upeo wa macho ya wazazi, alikuwa akijitoma kwenye mashamba ya majirani kujichumia!
Baada ya kupata staftahi yake ambayo kwa kweli ilikuwa chai ya mkandaa, alivaa mavazi yake ya kawaida na kujiambia kwamba leo atamngojea mwenzake njiani waucheze 'mchezo' wake wa kawaida.
Alipofika kwenye njia panda alivua sare yake ya shule na kubaki na vazi la ‘kazi’. Mwanafunzi mwenzake kwa jina Karaha alijiunga naye na baada ya Tandu kumweleza kuwa alichelea kuongezewa adhabu na mwalimu mkuu, walikata shauri kulitembelea shamba la mwalimu mkuu ambalo lilikuwa mkabala na shule yao.
Shamba hili lilikuwa limeshiba miti iliyozaa matunda ya kila aina. Tundu, mate yalimdondoka alipokuwa akiyatundulia macho matunda haya. Umaskini wa familia yake ulisahaulika machoni pa utajiri huu asioulalia wala kuuamkia. Walinyata kimya kimya katikati ya miti hii, manyezi yakimkumbatia Tundu kwa nguvu. Hii haikuwa mara yake ya kwanza kufaidi jasho la wengine, hivyo hakusita kujiuliza sababu ya uoga huo. Jambo ambalo Tundu hakutambua ni kwamba siku yake ya arubaini ilikuwa inabisha hodi.
Haukupita muda mrefu baada ya kuanza kuyatunda matunda kabla ya kusikia mrindimo wa nyayo.
Karaha, ambaye hakuwa mzoefu wa vitimbi vya Tundu, alitoa macho pima kwa uoga. Tundu aliendelea kufurahia kiamsha kinywa chake hadi pale alipotahamaki kuguswa begani. Alipogeuka alijikuta ametazamana ana kwa ana na mwenye shamba. Tundu alishikwa na kitetemeshi asijue la kufanya. Alipoulizwa sababu ya tabia yake hii, alisema kwamba wazazi wake maskini hawakumudu kumtimizia mahitaji yake ya kimsingi.
Karaha naye aliachama asijue la kufanya.
Mkuu wa shule alisikitishwa sana na kitendo cha wanafunzi hawa. Alimshauri Tundu aache tabia hii na kuyazingatia masomo yake Zaidi. Alimwonya Karaha dhidi ya kuwa bendera ambayo daima hufuata upepo.Aliwarudisha vijana hawa shuleni na baada ya kushauriana na walimu, alifanya mpango wa kumtafutia Tundu mshauri wa kumsaidia kurekebisha tabia yake.

41. Siku hii ilifanana na zingine za awali kwa sababu:
A. Tundu aliamka akiwa mchovu
B. Usiku uliotangulia ulikuwa na mambo mengi
C. Usiku uliotangulia hakuepuka adhabu
D. Tundu hakutarajia kupata lolote jema.

42. Maana ya neno 'ulizongwa' ni:
A. Ulijawa
B. Uliingiwa
C. Ulishikwa
D. Ulivamiwa

43. Kulingana na kifungu:
A. Aliyekosa kufanya mazoezi kila mara alipata adhabu mbili
B. Kulikuwa na wanafunzi wachache mno wenye tabia kama ya Tundu
C. Tundu hakupenda kufanya kazi yake shuleni
D. Adhabu aliyopewa Tundu siku hii alikuwa ameizoea.

44. Tundu alichelea kutoka kitandani kwa sababu
A. Hakuwa amekamilisha kazi hivyo alimwogopa mwalimu mkuu
B. Alikuwa mtovu wa nidhamu
C. Aliogopa kuongezewa kazi na mwalimu
D. Hakuwa mwenye adabu hivyo aliogopa kuadhibiwa na mwalimu mkuu.

45. “…….alivaa mavazi yake ya kawaida” ina maana
A. Alivaa nguo na magwanda yake ndani
B. Alivaa nguo na magwanda ya kawaida
C. Alivaa sare na magwanda yake ndani
D. Alivaa sare na nguo za nyumbani.

46. Maana ya “waucheze ‘mchezo’ wake wa kawaida” ni:
A. Wavae magwanda yao ya kawaida
B. Waibe katika mashamba ya majirani
C. Watoroke tena kutoka shuleni
D. Walivamie shamba la mwalimu mkuu.

47. Siku hii Tundu hakwenda shuleni kwa sababu
A. Hakutaka kupewa adhabu nyingine na mkuu wa shule
B. Hakutaka kupigiwa kelele na walimu
C. Alitaka kulipiza kisasi kwa mkuu wa shule
D. Mkuu wa shule alikuwa ameyaingilia mambo yake.

48. “Siku yake ya arubaini ilikuwa inabisha hodi” ina maana:
A. Uvivu wake ulikuwa karibu kugunduliwa
B. Mkuu wa shule alikuwa karibu kumwadhibu vikali
C. Mkuu wa shule alikuwa karibu kumpa onyo la mwisho
D. Uovu wake ulikuwa karibu kugunduliwa

49. Matendo yanayoonyesha kuwajibika kwa walimu ni
A. Kumrudisha Tundu shuleni, kumgusa begani, kumpa mashauri
B. Kumtimizia Tundu mahitaji, kumwadhibu, kumfumania
C. Kutoa adhabu, kutoa ushauri, kumrudisha Tundu shuleni
D. Kumsikitikia Tundu, kumrekebisha tabia, kumwonya.

50. Kulingana na kifungu
A. Karaha ana mazoea ya wizi
B. Karaha hana msimamo
C. Karaha aliadhibiwa na mwalimu
D. Karaha alirekebisha tabia.






More Question Papers


Popular Exams



Return to Question Papers