Get premium membership and access revision papers, questions with answers as well as video lessons.

Mathira District Mock- Kiswahili Paper 2 Question Paper

Mathira District Mock- Kiswahili Paper 2 

Course:Secondary Level

Institution: Mock question papers

Exam Year:2010



JINA: ____________________________________________________________
NAMBA YA MTIHANI _____________________
SAHIHI YA MWANAFUNZI ________________
TAREHE: _________________________________
102/2
KISWAHILI
KARATASI YA PILI
LUGHA
JULAI/AGOSTI 2010
MUDA - SAA 2 ½
MTIHANI WA PAMOJA - MATHIRA
MAAGIZO
a. Andika jina lako na namba yako katika nafasi ulizoachiwa hapa juu.
b. Jibu maswali yote. Majibu yako yaandikwe katika nafasi zilizoachwa katika kijitabu
hiki cha maswali.
A. UFAHAMU
Soma nakala kasha ujibu maswali
Huku tukiadhimisha siku ya kina Mama Duniani leo, kuna haja ya kutafakari
kuhusu nafasi ya wanawake katika jamii.
Kwanza kabisa tunafaa kufahamu mama ni nani. Mama ni mtu yeyote wa kike ambaye
hulea na kuionyesha familia na jamii mapenzi ya mama mzazi. Hii ina maana yeyote
anayeitimizia familia na jamii mahitaji haya awe dada, nyanya, shangazi, mfadhili, jirani
miongoni mwa wengine ni mama kwa mijibu wa mkutadha huu. Ni dhahiri kuwa mama
wamekuwa wakitekeleza majukumu muhimu maishani mwa familia na jamii lakini kama
punda, wengi wetu huishia kuwalipa kwa mateke.
Sio viongozi wa serikali, sio kina baba wala watoto: Miongoni mwao kuna wale
ambao wamejitolea kutowatambua na kutowaheshimu binadamu hawa wenye nguvu,
uwezo na maarifa yanayoandamana na mapenzi.
Kina mama na wanawake kwa jumla wamekuwa walengwa wakuu wa ghasia katika
familia na jamii.
Katika familia, kwa mfano, kina mama wengi mpaka leo wanapigwa na kuteswa
na wanaume zao bila sababu. Wengi wao wameachiwa jukumu la kuwalea watoto hata
baada ya kukubali mzigo huo mzito, wanachapwa kila siku.
Visa vya kina mama wanaorauka kila siku kwenda kutafutia wanao chakula na
wanaporudi wanaopigwa na waume wao kwa kizingizio cha kuzurura ovyo ni matukio ya
kila siku. Baadhi ya wanaume pia hukaa ndee kuwasubiri wake wao watafute na kisha
huwanyang’anya kibaba chao kuongezea kwa machozi.
Baadhi ya wanawake mpaka sasa wamesalia watumwa na waume amabo hutoa amri na
hawatarajii maswali wala manung’uniko.
Haki za ndoa za kina mama zinaendelea kuvunjwa na mabwana zao ambao
wamejigeuza madubwana.
Pili, watoto, hasa wa kiume, ambao huingiwa na kasumba za dhuluma kutoka kwa
baba na jamii pia wamekuwa wakiwakosea kina mama heshima bila kujali. Sio mara
moja au mbili nimesikia na hata kushuhudia kina mama wakipigwa na watoto wao wa
kiume baada ya mzozano.
Watoto wa kiume wamejaa utundu, kwa mfano, ni mzigo mkubwa kwa kina mama mbali
na kuwa tishio kwa furaha na amani yao katika familia na jamii.
Wengi wa watoto hao hukataa shule na kujiunga na magenge ya wahuni ambayo hutumia
dawa za kulevya na kila baada ya kulewa wao huishia kuwachokoza mama zao.
Baadhi yao hutaka mambo yasiowezekana na kukosa kufanya wanachotaka huwa ni
matusi na kichapo cha mbwa kwa mama.
Viongozi wa serikali na kisiasa pia wamekuwa wakijikosea heshima kwa kuendeleza
mateso ya kina mama. Baadhi yao hudai wanawake hawana haki ya kuongea mbele yao
huku wengine wakiwashambulia wakati wa kampeni.
Maswali
a. Pendekeza kichwa mwafaka cha taarifa hii. (alama 1)
b. Kwa mujibu wa kifungu, ni nani anastahili kuitwa mama. (alama 3)
c. Ni matatizo gain yanayowakabili akina mama. (alama 4)
d. Taja makundi mbali mbali yanayonyanyasa akina mama. (alama 3)
e. Eleza kwa nini mwandishi anafananisha kina mama na punda. (alama 2)

f. Elelza maana ya maneno haya kama yalivyotumiwa katika kifungu. (alama 2)
i. Mfadhili
ii. Madubwana
B. UFUPISHO
Binadamu hupambana na mazingira yake katika harakati za kujaribu kutosheleza
mahitaji yake ya kila siku. Katika hali hii ya mapambano, mambo mengi mapya
hufichuka. Mambo haya huwasaidia binadamu kuelewa zaidi na kuyadhibiti mazingira
anamoishi.
Hali hii ya mtu kupambana na mazingira yake kwa minajili ya kujikimu
imemwezesha kupiga hatua kubwa katika nyanja za kijamii, kiuchumi, kisiasa na
kiteknolojia. Mwanadamu ameweza kuvumbua vitu mbali mbali vya kuboresha maisha
yake ikiwa ni pamoja na utendaji kazi. Kwa mfano, kuibuka kwa mfumo wa teknolojia
ya mawasiliano unaotumia mitambo ya kompyuta ili kuunda mtandao wa mawasiliano ni
njia mojawapo ya kuimarisha maisha ya mwanadamu. Teknolojia hii imepunguza
masafa ya ulimwengu na kuifanya dunia kuonekana kama kitongonji kidogo ambapo mtu
aliye mashariki ya mbali anaweza kusabahiana kwa wepesi na mtu ambaye yuko nchini
Kenya.
Kupitia kwa mtandao, unaweza kujua gharama za bidhaa katika sehemu mbali
mbali ulimwenguni. Huduma za malipo kwa bidhaa kama hizo pia zimeimarishwa. Pesa
zinaweza kusafirishwa kwa haraka zaidi kupitia kwa mtandao hata kama mtu haweki
akiba benki. Wafanyi biashara nao wanaweza kupata huduma za benki bila kumlazimu
kwenda katika tawi lake. Huduma za benki na mabadilisho yoyote ya pesa yanaweza
kufanyika kupitia kwa mtandao. Ustaarabu huu pia umemwezesha mwanadamu kupata
habari za pembe zote za ulimwengu pindi zinapochipuka. Wengine wameweza kupata
wachumba kupitia kwa mtandao wa mawasiliano. Maendeleo haya ya kiteknolojia pia
yanaweza kukuza uwezo wa kijeshi wa nchi mbalimbali. Mwanadamu ameweza kuunda
zana changamano za kujihami pamoja na silaha za maangamizi makubwa kama vile
silaha za kinyuklia na zile za kitonoradi.
Hata hivyo, hakuna jema lisilokuwa na dosari. Maendeleo haya yana madhara
yake. Kwa mfano, silaha hizi za nyuklia ni tisho kubwa kwa maisha ya mwanadamu,
wakati mwingine nchi hujiingiza kwa vita ovyo bila sababu ya maana. Ustarabu wa
mtandao wa mawasiliano umesambaratisha misingi ya utamaduni wa nchi zinazoendelea.
Nchi hizi zimeathiriwa pakubwa kutokana na utamaduni wa kigeni kama vile desturi za
ulawiti, misago, mapenzi ya mtandao, mavazi ya nusu uchi na kutothamini ndoa, badala
yake kuridhia kuzaa nje ya ndoa na kutukuza jamii ya mzazi mmoja. Mambo haya
yamechangia kuwepo kwa ukahaba katika jamii. Maendeleo ya viwanda yameathiri
mazingira ya mwanadamu vibaya kwa kusababisha uchafuzi wa hewa, maji na uharibifu
wa misitu ambazo ni raslimali muhimu kwa nchi licha ya kwamba misitu huileta mvua na
kuchuja hewa.
Hata hivyo, maendeleo haya ya kiteknoljia ya mawasiliano yakitumiwa kwa
uangalifu yataimarisha hali ya maisha ya mwanadamu na hupafanya hapa duniani mahali
pazuri pa kuishi.
Maswali
a. Teknolojia ya mawasiliano ina manufaa gain ya maendeleo? Tumia maneno 45 –
50. alama – 8
Utiririko - 1
b. Eleza madhara yanayotokana na maendeleo ya kiteknologia. Tuumia maneno 40.
(alama 5) (Utiririko 1)
C. MATUMIZI YA LUGHA
a. Yaweke maneno haya katika ngeli zake.
i. Tepe _________________________________ (alama 1)
ii. Uasi _________________________________ (alama 1)
b. Tambua aina za vitenzi katika sentensi ifuatayo.
Juma alikuwa angali mkulima. (alama 1)
c. Ainisha aina za viambishi katika kitenzi ‘iliwawia’ (alama 2)
d. Yakinisha sentensi ifuatayo
Yohana alipolala jana hakuota. (alama 1)
e. Tunga sentensi ukitumia kiunganishi ‘ilihali’. (alama 1)
f. Sahihisha sentensi ifuatayo.
Ningelikuwa mwanafunzi ningalisoma kwa bidii. (alama 1)
g. Andika sentensi ifuatayo katika kauli ya kutendama. (alama 1)
Serikali ina mambo mengi ambayo yamefichwa
h. Kihisishi kilichotumika katika sentensi ifuatayo ni cha aina gain? (alama 1)
“Yarabi! Leo unanipita hivi hata hali huniulizi? Kuna nini jamani?”
i. Eleza matumizi ya kwa katika sentensi ifuatayo. (alama 1)
Kucheza kwa Mariga kumewafurahisha wakenya.
j. (i) Eleza maana ya sentensi changamano. (alama 1)
(ii) Toa mfano mwafaka. (alama 1)
k. Tambua aina ya shamirisho kitondo katika sentensi hii. (alama 1)
Kabi alimrushia Maimuna mpira.
l. Geuza senetensi hii iwe katika usemi wa taarifa. (alama 2)
“Wageni wetu mliofika hapa, mko huru kujionea maendeleo ya nchi yetu,”
waziri akatamka.
m. Tunga sentensi moja ukitumia kitenzi-nomino. (alama 1)
n. Dhihirisha matumizi ya “ndi” katika sentensi ifuatayo. (alama 1)
Sisi ndisi wenye shamba hili.
o. Chorea mishale sentensi ifuatayo. (alama 4)
Mimi sikumwona wala kumsikia.
p. Sauti _e_ na _u_hutamkwa vipi? (alama 1)
q. Tambua viwakilishi nafsi katika neno hili. (alama 1)
Alimgonga
r. Onyesha kirai kivumishi katika sentensi ifuatayo. (alama 1)
Tulipoenda sokoni, tulikutana na wanabiashara mashuhuri.
s. Andika kwa ukubwa. (alama 1)
Mlima una msitu mkubwa.
t. Akifisha kifungu kifuatasho. (alama 3)
nilipoitwa na nyanyangu ili anitume dukani alinitazama halafu akaniuliza
kweli wewe ni mwaminifu
u. Andika kwa kinyume. (alama 1)
Nyanya alifumbua fumbo.
v. Onyesha aina za vishazi katika sentensi ifuatayo. (alama 2)
Rais aliwasihi waisome katiba kabla ya kufanya uamuzi.
w. Tumia kiwakilishi ‘o’ rejeshi katika hali ya mazoea. (alama 1)
Kasisi hutuambia mambo ambayo hueleweka.
x. Unda nomino moja kutoka kwenye kitenzi kifuatacho. (alama 1)
-fa
y. Eleza maana mbili za sentensi ifuatayo. (alama 2)
Mtoto anapendezwa na ziwa.
z. Andika neno lenye maana sawa na, (alama 1)
Uchechefu
D. MATUMIZI YA LUGHA
(a) Taja lahaja zozozte za Kiswahili (alama 2)
(b) Eleza sababu tatu zinazochangia kuzuka kwa wingilugha nchini. (alama 3)
(c) Eleza juhudi zozote tano zinazowasaidia kuboresha luugha ya Kiswahili nchini.
(alama 5)






More Question Papers


Popular Exams



Return to Question Papers